Ninayo furaha kubwa kukuletea ndugu msomaji wa maelezo juu ya fursa za uwekezaji zilizopo Halmashauri ya Wilayani ya Nkasi kwa malengo ya kukuwezesha kuifahamu vema wilaya yetu pamoja na fursa mbalimbali tulizojaliwa wilayani ambazo zinawezesha uwekezaji wa aina mbalimbali katika maeneo yote yanayohusiana na maendeleo ya kiuchumi na kijamii pia. Halmashauri ya Wilayani ya Nkasi imejaliwa kuwa na rasilmali nyingi za asili ambazo bado hazijawekewa uwekezaji wa kutosha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu na/au upungufu wa mitaji ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji mkubwa na ule wa ngazi ya kati. Aidha, uwekezaji katika Halmashauri yetu bado ni wa chini kutokana na wawekezaji wengi ha hasa wale wenye mitaji mikubwa kutokuwa na taarifa sahihi na/au kutokuwa na taarifa kabisa juu ya fursa zilizopo kwamba wangekuja kuwekeza W Halmashauri ya Wilayani ya Nkasi. Uwekezaji mkubwa katika Halmashauri yetu ni mojawapo ya njia madhubuti zinazoweza kupunguza na kama si kuutokomeza kabisa umaskini katika halmashauri ya wilaya na hivyo kutimiza maono ya maendeleo ya Tanzania ifikapo mwaka 2025.
Wilaya ya Nkasi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa ujumla ilianzishwa mnamo mwaka 1983 na ina jumla ya tarafa 5, kata 28, vijiji 93 na vitongoji 762 Wilaya ina waheshimiwa wabunge 2 wanaowawakilisha wananchi katika majimbo mawili ya uchaguzi yaliyopo ambayo ni; Nkasi Kaskazini, na Nkasi Kusini. Wilaya pamoja na vyombo vingine vya kiutendaji vilivyopo inaendeshwa kupitia Halmashauri ya wilaya ambayo ina jumla ya waheshimiwa madiwani 42 ambapo madiwani 28 ni wa kuchaguliwa na madiwani 14 ni wa viti maalum.
Nkasi na mojawapo ya wilaya 3 zinazounda mkoa wa Rukwa. Kijiografia, Wilaya ya Nkasi ipo katika nyanda za juu kwa urefu wa wastani wa mita 1,700 kutoka kwenye usawa wa bahari na inapakana na wilaya ya Kalambo na Sumbawanga vijijini zilizopo upande wa kusini mwa wilaya, na upande wa kaskazini wilaya inapakana na wilaya ya Mpanda vijijini, na upande wa mashariki inapakana na wilaya ya Mlele; wilaya hizi mbili zipo mkoa wa Katavi. Lakini pia, wilaya ya Nkasi inapakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa magharibi kwa kutenganishwa na Ziwa Tanganyika.
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ina ukubwa wa kilometa za mraba 13,124 ambapo; kilometa za mraba 9,375 ni ardhi na kilometa za mraba 3,749 ni maji. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi (2012) Wilaya ya Nkasi ina jumla ya watu 281,200 ambapo; wanaume ni 137, 788 na wanawake ni 143,412. Wastani wa Halmashauri ya Wilaya wa ukubwa wa kaya ni watu 5.
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imejaliwa kuwa na hali nzuri ya hewa kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali. Mvua zinazonyesha kwa mwaka hunyesha kwa wastani wa mililita 750 hadi 1,200 na kwa kawaida huanza katikati ya mwezi Novemba na hukatika katikati ya mwezi Aprili au Mei mwanzoni. Udongo uliopo Halmashauri ya Wilaya wenye rutuba na huwezesha kustawisha mazao ya aina mbalimbali ikiwemo mahindi, maharage na jamii nyingine zote za mikunde, muhogo, viazi vya aina zote, karanga, alizeti, mpunga, ulezi, miwa, ufuta,
Ardhi yenye rutuba kwa malisho pamoja na hali nzuri ya hewa inawezesha pia kustawi wa mifugo ya aina mbalimbali Wilayani. Hali hii imesaidia sana kustawisha mifugo yenye afya bora na kwa viwango vya kimataifa; kwa mfano, wilaya sasa inafuga na kuzalisha mifugo aina mbalimbali kutoka nchi za nje ya Santa gertruids kutoka Afrika ya Kusini, Germany simmented kutoka Ujerumani. Aina nyingine za ng’ombe waliopo wilayani ni boran, zebu, na wale wa asili wa Kifipa. Kwa ujumla, kuna zaidi ya ng’ombe wa kisasa wa nyama 33,400 wenye thamani ya zaidi ya USD. 10m wanaofugwa wilayani na wafugaji wapatao 200 chini ya Mpango kabambe wa Wilaya wa Maendeleo ya Mifugo. Mafanikio ya Mpango huu ni pamoja na kuiletea Wilaya ushindi wa Kwanza wa kumpata ng’ombe bora na mfugaji bora wa kikanda-Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Kitaifa mfululizo kwa mwaka 2011, 2012, 2013, na 2014.
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imejaliwa kuwa na sehemu kubwa ya Ziwa Tanganyika; urefu wa kilometa .......... kutoka kijiji cha Kalila upande wa kaskazini hadi kijiji cha Kilambo cha Mkolechi kilichopo kusini mwa wilaya. Ziwa Tanganyika linasifika kwa kuwa ziwa refu na lenye kina kirefu lililo na samaki na dagaa wa kipekee duniani. Ziwa hili linatoa fursa kubwa, nyingi na za kipekee kabisa za uwekezaji kuanzia zile za uzalishaji wa mazao ya ziwa na utalii wa kimataifa.
Halmashauri ya Wilaya imekabiliana na changamoto ya miundombinu duni ya mawasiliano na nishati jambo lililokuwa linatishia uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali wilayani. Changamoto hii sasa itakuwa historia kwani ujenzi unaoendelea na upo katika hatua za mwisho wa barabara ya lami itokayo Mbeya kupitia wilayani Nkasi hadi Mpanda itaimarisha usafiri na usafirishaji wilayani. Umeme wa kampuni ya Tanesco, na huduma za mawasiliano ya simu, wavuti na tovuti zinazotolewa na makampuni ya Voda, Tigo, Tccl, Airtel, Zantel vipo na usambazaji kwenda kwenye maeneo ya vijijini unaendelea.
Kwa ujumla, fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii Halmashauri ya Wilaya ni nyingi kwamba hakuna maana tena ya wawekezaji kusita kuja kuwekeza kwenye Halmashauri yetu. Taarifa hii fupi imetayarishwa maalum kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ili kwa pamoja tuweze kuuinua uchumi wetu na hivyo kupata maendeleo. Iwapo mtu unayo ndoto ya kuwekeza ili uweze kupata maendeleo thabiti, basi mahali sahihi panapoweza kutimiza ndoto yako ni kuja kuwekeza Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Karibu Wilayani Nkasi!
Nkasi District Council
Anwani ya posta: P. O. Box 2, Namanyere - Nkasi
Simu: +255252830006
Simu ya mkononi: +255252830006
Barua pepe: ded@nkasidc.go.tz
Haki miliki