Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dr.Edwin Mhede amezindua chanjo ya mifugo Julai 8 2025 zinazotolewa kwa Ruzuku ya Serikali Kimkoa katika Ranchi ya Kalambo iliyopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Katika Mkoa wa Rukwa.
Naibu Katibu Mkuu huyo amezindua Chanjo ya Ugonjwa wa Homa ya Mapafu kwa ng'ombe (Contagious Bovine Pleuropneumonia-CBPP) ambayo itatolewa kwa nusu ya bei halisi ambapo mfugaji atachangia shilingi 500 tu kwa dozi ya ng'ombe mmoja.Utoaji wa Chanjo hii utaenda sambamba na utambuzi kwa njia ya heleni ambayo itatolewa bila malipo kwa kila ng'ombe atakayechanjwa.
Hata hivyo Mhede amezindua Chanjo ya tatu moja kwa kuku ambayo inazuia magonjwa matatu kwa wakati mmoja ambayo ni Mdondo/Kideri,Ndui ya Kuku na Mafua ya kuku yanayoambukiza ambayo itatolewa kwa Ruzuku ya Serikali kwa asilimia 100.
Akihutubia wananchi Mheshimiwa naibu Katibu Mkuu alieleza wananchi wajitokeze kuleta mifugo yao kwenye vituo vya chanjo kwani chanjo hizi ni Salama na zitakinga mifugo yetu dhidi ya magonjwa ambayo yanasumbua sana mifugo hapa nchini na hivyo kuongeza uzalishaji na tija ya Ufugaji.
Aliongeza mifugo yetu itakapochanjwa itakuwa na afya bora hali itakayoongeza fursa zaidi katika masoko ya nje na kuongeza kipato cha mfugaji na Taifa kwa ujumla hivyo tujitokeze tukachanje mifugo yetu maana "ujanja ni kuchanja mifugo" Alisisitiza wataalam kukamilisha zoezi la chanjo kufikia Oktoba 2025.
Nkasi District Council
Anwani ya posta: P. O. Box 2, Namanyere - Nkasi
Simu: +255252830006
Simu ya mkononi: +255252830006
Barua pepe: ded@nkasidc.go.tz
Haki miliki