WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO KWA WATUMISHI WA HALMASHAURI NCHINI.
Imewekwa tarehe: December 17th, 2022
Awataka kwenda vijijini kuwasikiliza wananchi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi kwenye Halmashauri zote nchini kutenga muda wa siku tatu kati ya siku za kazi kwenda vijijini ili kutatua changamoto za wananchi.
Amesema kuwa ni lazima watumishi wa umma wajue wajibu mkubwa ni kuwatumikia wananchi na kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao.
Amesema hayo Disemba 16, 2022 wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa umma wa Halmashauri za mkoa Rukwa ambako alikuwa kwenye ziara ya kikazi.
Amesisitiza kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona kila mtumishi wa umma anawajibika katika kuwatumikia watanzania “Hawa wananchi wamesambaa katika Wilaya na halmashauri, tumejenga majengo ya ofisi sio lazima wananchi waje humo kupata huduma, wapo wengine hawawezi kuja hapa lakini wanahitaji Serikali yao inahudumie”
Aidha, Mheshimiwa amewataka viongozi katika halmashauri kuhakikisha wanasimamia watumishi kutokaa ofisini wiki nzima badala yake waende vijijini kwani huko ndiko wananchi walipo ili wawasikilize na kuwatumikia.
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu amewataka watumishi wanaosimamia eneo hilo kufanya makadirio yenye uhalisia na kutambua vyanzo vyote ambavyo vinaweza kuingiza mapato “lazima mfanye tathmini eneo fulani linaweza kuwaingizia kiasi gani, kwa siku, kwa mwezi au kwa mwaka”
“Tunapotaka kukusanya mapato ya ndani anzeni kwa kubaini vyanzo na msiwaachie wakuu wa idara pekee “ Meya na wenyeviti wa halmahauri tushiriki kikamilifu, watendaji wa vijiji na kata hata watumishi wengine, tukishabaini turudi kusimamia sote”
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia amewekea nguvu katika eneo la makusanyo “hakuna haja ya kutumia nguvu kubwa katika hili muhimu ni kusimamia, Serikali imeagiza kukusanya kielektroniki, tufanye hivyo, tumieni mashine zetu za POS”