MKOA RUKWA WAZINDUA MPANGO MAKAKATI KUDHIBITI MAAFA.
Nkasi – Rukwa
Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na ofisi ya waziri mkuu imezindua mpango mkakati wa usimamizi wa maafa ambao utasaidia kupunguza viashiria vya maafa ambayo yamekuwa yakijitokeza kila mwaka kwa kuharibu miundombinu ya serikali na makazi ya wananchi.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa mpango huo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. James Kilabuko wilayani Nkasi mkoani Rukwa, amesema mpango huo utasaidia katika usimamizi wa maafa katika Halmashauri zote za mkoa huo, huku akisisistiza nyaraka hizo kutekelezwa kwa vitendo.
Aidha ameongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji wa tahadhari ya awali, kujenga uwezo wa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Eliudi Njongellah ,amesema mpango huo umekuja katika wakati muafa ambapo Halmashauri imekuwa ikikabiliwa na maafa yanayosababishwa na majanga hasa ya Upepo Mkali, Magonjwa ya Mlipuko kwa binadamu na wanyama, mafuriko pamoja na mgongano wa wanyamapori na binadamu ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na kwamba uwepo wa makakati huo utasaidia kuimarisha uwezo wa wananchi kupanda miti kwenye maeneo ya makazi.
Licha ya hilo, amesema uandaaji wa nyaraka za usimamizi wa maafa ni hatua nzuri kueleka katika ujenzi wa jamii iliyo stahimilivu dhidi ya majanga katika Wilaya ya Nkasi, hivyo ni wajibu wa kila Idara, Vitengo na Taasisi zote zilizopo katika Halmashauri, kuzingatia dira katika kutekeleza vipaumbele vya kisekta.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Brigedia Generali Hosea Ndagala, amesema Idara hiyo imekuwa ikichukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mheshimiwa Peter Lijualikali ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu na shirika la kuhudumia Watoto ulimwenguni (UNICEF), kwa kazi nzuri ya uandaaji wa nyaraka za usimamizi wa maafa na kutoa elimu juu ya masualsa ya menejimenti ya maafa kwa Wilaya ya Nkasi na kuahidi kuzifanyia kazi nyaraka hizo ili kuleta matokeo chanya.
Nkasi District Council
Anwani ya posta: P. O. Box 2, Namanyere - Nkasi
Simu: +255252830006
Simu ya mkononi: +255252830006
Barua pepe: ded@nkasidc.go.tz
Haki miliki